11 Mei 2025 - 18:11
"Kuna Wivu wa Husuda na Wivu Ghibta | Je, Tuwe na Wivu wa Aina ya Ghibta au Tusiwe nao?"

Husuda ni kutamani neema ya mtu mwingine itoweke, iwe neema hiyo itamfikia mwenye husuda au la. Kinyume cha husuda ni 'Ghibta', ambapo mtu hatamani neema ya mwingine ipotee, bali anatamani kuwa na neema kama hiyo bila kumtakia mwingine mabaya.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-: Swali: "Ninapowaona marafiki zangu wakipiga hatua, ninahisi huzuni na najilinganisha nao! Je, nina husuda?".

"Kuna Wivu wa Husuda na Wivu Ghibta | Je, Tuwe na Wivu wa Aina ya Ghibta au Tusiwe nao?"

Jawabu kwa Muhtasari:

Hapana, si kila huzuni au kujilinganisha na mafanikio ya wengine ni husuda. Hali hiyo inaweza kuwa ni wivu wa aina ya ghibta (wivu mzuri), hasa kama hutamani mabaya kwa marafiki zako, bali unahisi wewe pia unapaswa kufanikiwa kama wao.

Jawabu kwa Ufafanuzi zaidi:

Sifa za kimaadili—ikiwa ni nzuri au mbaya—ndizo zinazojenga msingi wa mafundisho ya maadili. Kati ya sifa hizi, baadhi ni za msingi na zinaathiri tabia nyingine nyingi. Husuda (wivu mbaya) ni mojawapo ya sifa mbaya zilizokemewa sana, kwa sababu huwa ni kiini cha maovu mengine mengi. Ili kutofautisha husuda na sifa zinazofanana nayo kama الغِبْطَةُ / Ghibta (wivu mzuri), hebu tuchambue maana zake:

1. Maana ya Husuda na Ghibta:

Husuda (kwa Kifarsi huitwa "رشك") ni hali ya kutamani neema au baraka aliyo nayo mtu mwingine iondoke, iwe hiyo neema itamfikia mwenye husuda au la. Kwa hivyo, mwenye husuda huwa kama mharibifu wa moyo—hataki kuona watu wakibarikiwa na Mwenyezi Mungu, hata kama yeye hatapata kitu hicho.

Ghibta, ni kinyume chake, ni kutamani kuwa na neema kama ya mwingine bila kutamani ipotee kwake. Ni aina ya motisha chanya inayoweza kumchochea mtu kujiendeleza bila chuki au choyo(1).

Nukuu kutoka kwa Maimamu:

Katika hadithi kutoka kwa Imamu Ja‘far as-Sadiq (a.s), inasemwa:

(“إِنَّ الْمُؤْمِنَ يَغْبِطُ وَلَا يَحْسُدُ، وَالْمُنَافِقَ يَحْسُدُ وَلَا يَغْبِطُ”).

"Muumini huwa na ghibta lakini hahusudu, na mnafiki huhusudu lakini hana ghibta"(2).

Hii inaonyesha kuwa ghibta ni tabia inayokubalika kwa Muumini, kwa sababu haileti uharibifu wa kijamii au wa moyoni, tofauti na husuda ambayo ni sumu ya roho.

Kwa hiyo:

Ikiwa unahisi huzuni unapoona mafanikio ya wengine lakini hutamani wapoteze hayo mafanikio, basi hiyo ni ghibta, si husuda. Hali hii ni ya kawaida, lakini inapaswa kugeuzwa kuwa motisha ya kujitahidi zaidi, si chanzo cha huzuni ya kudumu.

Ikiwa unahisi huzuni hiyo inakuletea chuki, unyonge, au kutaka mtu mwingine apoteze alicho nacho, basi hiyo inaweza kuwa dalili ya husuda, na inapaswa kutibiwa kimaadili na kiroho.

Kwa mujibu wa Faydh al-Kāshānī:

"Tambua kuwa husuda huihusu neema, na kila mara Mwenyezi Mungu anapomruzuku nduguyo kwa neema, wewe unaweza kuwa na mojawapo ya hali mbili:

Kwanza: Unachukia hiyo neema na unatamani ipotee—hii ndiyo husuda. Husuda humaanisha kumchukia mwenye neema na kutamani apokwe (neema hiyo) hata kama wewe hautapata hiyo neema.

Pili: Hutaki hiyo neema ipotee, wala huumii kuiona ikiendelea (kwa nduguyo), lakini unatamani kuipata pia kwa upande wako—hii ndiyo Ghibta" (3).

____________________________________

2. Kutofautisha Husuda na Ghibta kwa Vitendo

Kwa maelezo hayo, kila mtu anapaswa kujiangalia na kujiuliza:

• Je, natamani neema za watu zipotee?!.

• Au natamani kuwa na neema kama wao, bila wao kupoteza walicho nacho?.

✅ Ikiwa unatamani kuwa kama wao bila wao kuathirika, hiyo ni Ghibta – haina kosa (wala ubaya wowote).

❌ Lakini kama unafurahia wakishindwa au kupoteza mafanikio yao, hata kama hutafaidika (na mafanikio hayo huyapati wewe, unatamani tu wakose na waondokewe na kila walichokuwa nacho), hiyo ni husuda, na inahitaji tiba ya maadili na kiroho.

____________________________________

3. Uchungu wa Ndani na Kujisikitikia

Wakati mwingine mtu huumizwa kiroho au kihisia anapoona wengine wakiwa na neema, bila hata kutamani wapoteze na kuondokewa na neema hizo, wala kutamani kuwa kama wao.

Hii ni hali ya kujichoma moyoni, kujilinganisha (na wengine) kupita kiasi, na kutojiridhisha, hata kama si husuda wala Ghibta.

🔻 Hali hii si nzuri kiakhlaki, kwani:

• Huchafua roho ya mtu.

• Huondoa furaha na utulivu wa ibada.

• Hupunguza hali ya kiroho na uhusiano na Mwenyezi Mungu.

____________________________________

Hitimisho:

Husuda ni tabia mbaya kabisa, na ni chanzo cha maovu mengi katika jamii. Na maana ya Husuda: Ni kutamani neema ya mwingine ipotee, hata usiponufaika (wewe binafsi kwa kupotea neema yake).

Ghibta ni kutamani kuwa na neema kama ya mwingine bila kumtakia mabaya – hii inakubalika na huweza kuchochea maendeleo (ya mtu katika jamii).

Kuna hali ya tatu: Huzuni ya moyoni (mtu kuumia au kihisia ndani kwa ndani, yaani anachomeka moyoni kwa kuoona neema za wengine) bila husuda au Ghibta, hii nayo nayo si nzuri – ni sumu ya ndani inayodhuru maisha ya kiroho.

🟢 Suluhisho ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Hekima, na kutafakari juu ya neema alizokupa binafsi, kisha kuwa na shukrani daima.

_

Asante sana kwa kufaidika na somo hili fupi.

Karibu tena.

Imeandikwa na: Sheikh Taqee Zachalia Othman.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha